Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Dkt. Grace Ntogwisangu, amesisitiza umuhimu wa utoaji wa chanjo kwa haki na kwa kuzingatia matumizi ya teknolojia ya kisasa ili kuzuia magonjwa ya mlipuko na kuboresha huduma za afya kwa wananchi.

Akizungumza leo tarehe 4 Februari, 2025 wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa chanjo (ITMR na Gothomis) yaliyofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Dkt. Ntogwisangu amesema matumizi sahihi ya mifumo hiyo yataongeza ufanisi, uwazi na usahihi katika utoaji wa huduma za chanjo katika vituo vya afya.

Ameeleza kuwa ni muhimu kwa kila mhudumu wa afya kuwa tayari kupokea na kutekeleza mafunzo hayo kwa vitendo ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya afya, akisisitiza kuwa zoezi hilo linapaswa kutekelezwa bila vikwazo.

“Chanjo ikitendewa haki, tunaepuka magonjwa ya mlipuko. Ni muhimu kwenda sambamba na teknolojia ili kuhakikisha huduma bora za afya zinatolewa kwa wananchi,” amesema Dkt. Ntogwisangu.

Kwa upande wake, Msimamizi wa Mafunzo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Bi. Joseline Samson Ishengoma, amewataka washiriki wa mafunzo hayo kujifunza kwa umakini na kuhakikisha wanayatumia maarifa waliyopata katika maeneo yao ya kazi.

Bi. Ishengoma amesema utekelezaji mzuri wa mafunzo hayo utasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za chanjo pamoja na kuboresha ukusanyaji na usimamizi wa taarifa za afya kwa kutumia mifumo ya kielektroniki.

Mafunzo hayo yamewakutanisha wataalamu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu - TAMISEMI, Wizara ya Afya na Mpango wa Chanjo ya taifa pamoja na watoa huduma za chanjo kutoka vituo vyote vya afya vya Wilaya ya Ikungi, yakiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha huduma za chanjo zinaboreshwa kwa kutumia teknolojia ya kisasa.

Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa