Leo tarehe 30 Januari, 2026, Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi limeendelea na siku ya pili ya kikao chake kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri.

Akifungua kikao hicho, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Mheshimiwa Ally Juma Mwanga, amewakumbusha Madiwani kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo, hususan wao kama wenyeviti wa kamati za maendeleo ya kata.

Amesisitiza umuhimu wa usimamizi wa karibu wa miradi hiyo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Mwenyekiti Mwanga amebainisha zahanati zilizopo katika hatua za mwisho za ukamilishaji na kusisitiza zisimamiwe kwa karibu ili huduma za afya zianze kutolewa kwa wananchi. Zahanati hizo ni Unyampembe, Mtavira, Nkuninkana, Msule, Mduguuyu, Samaka na Makonda.

Amesema kuwa ni dhamira ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuona wananchi wanapata huduma bora, hivyo amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kuhakikisha fedha zilizotengwa kwa ajili ya kukamilisha miradi hiyo, hususan ya sekta ya afya, zinatumika haraka na kwa ufanisi.

Wakati wa kufunga kikao hicho, Mwenyekiti Ally Mwanga aliwashukuru wajumbe wote wa Baraza kwa ushiriki wao mzuri na kutoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji kuongeza upatikanaji wa mbegu za mazao ya muda mfupi yanayotumia maji kidogo, ili kuwasaidia wakulima kukabiliana na changamoto ya upungufu wa mvua. Aidha, aliagiza matrekta yaliyotolewa na serikali yatumike mashambani kwa utaratibu uliowekwa, yakodishwe kwa bei nafuu kama ilivyoelekezwa, badala ya kubaki bila kutumika.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Bi. Haika Massawe, alimshukuru Mwenyekiti na Baraza la Madiwani kwa ushirikiano wao na kuahidi kuwa maelekezo yote yaliyotolewa yatafanyiwa kazi kwa haraka ili kuendelea kuimarisha maendeleo ya Halmashauri.

Katika kikao hicho, Baraza pia lilipokea na kujadili maazimio ya Kamati za Kudumu za Halmashauri, ambazo ni Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango, Kamati ya Kudhibiti UKIMWI, Kamati ya Huduma za Uchumi pamoja na Kamati ya Huduma za Jamii.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa