SERIKALI imetoa trekta ndogo 34 aina ya Power Tiller kwa halmashauri tano za Mkoa wa Singida ambazo zitakuwazinakodishwa kwa wakulima kwa bei nafuu waweze kuongeza uzalishaji ili ifikapo 2030 lengo la kilimo kuchagia asilimia 10 ya pato la taifa liweze kufikiwa.
Katibu Tawala Msaidizi Mkoa wa Singida Sehemu ya Uchumi na Uzalishaji, Stanslaus Choaji, akizungumza juzi wakati wa zoezi la kugawa ambalo lilifanywa na Mkuu wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, alisema kuwa katika awamu ya kwanza Halmashauri za Wilaya ambazo zimepata mgao ni Halmashauri ya Wilaya Ikungi ambayo imepata Power Tiller 15, Mkalama 12, Singida DC 3, Iramba 2 na Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni imepata 2.
“Lengo la mpango huu wa serikali ni kufikisha zana za kilimo karibu na wakulima na kuwafanya wakulima waweze kupata huduma ya upatikaji wa zana za kilimo kwa bei nafuu ikilinganishwa na ile wanayokodi kwa watu binafsi hatimaye waweze kuongeza uzalishaji ili kufikia 2030 tuweze kufikia lengo la kilimo kuchangia asilimia 10 ya pato la taifa,” alisema.
Choaji alisema trekta hizo zitawekwa kwenye vituo vya zana za kilimo ngazi ya kata ambapo kutawekwa utaratibu wa namna ya kukodisha na kuwaomba wakulima kuhakikisha wanatumia zana hizo kuongeza maeneo ya kilimo ili waweze kulima kwa tija zaidi na kuongeza uzalishaji.
Alisema matarajio ya serikali ni kwamba baada ya wakulima kupata zana hizo uzalishaji utaongezeka maradufu ukilinganisha na ilivyo sasa kwasababu wakulima wataweza kuandaa mashamba mapewa kwa bei nafuu na pesa ambazo walikuwa wakizitumia kukodi matreka kwa watu binafsi sasa watazielekeza kununulia mbolea na mbegu za ruzuku.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida,Halima Dendego,akikabidhi ‘power tiller’ hizo kwa Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri za Wilaya, alisema baada ya kupata zana hizo jukumu liliobaki ni kuhakikisha kinazalishwa chakula cha kutosha pamoja na ziada kwa ajili ya kuuza ili kuongeza pato la kaya, mkoa na hatimaye pato la taifa.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa