Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, leo tarehe 15 Desemba 2025, amefanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Ikungi.
Kabla ya kuanza ziara hiyo, Dkt. Maganga alifanya kikao na Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, ambapo aliwataka kuhakikisha mapato ya Halmashauri yanaongezeka na kufikia malengo yaliyopangwa.
Aidha, amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kuhakikisha vijiji vyote 101 vinapewa POS za kukusanyia mapato ili kuziba mianya ya ukwepaji na upotevu wa mapato ya Serikali.
Katika kikao hicho, Dkt. Mganga pia alisisitiza kuwa ifikapo mwezi Machi 2026, zoezi la chanjo za mifugo liwe limekamilika katika maeneo yote ya wilaya hiyo.
Akizungumza kuhusu vyanzo vya mapato, alisema:
“Ili mapato yaongezeke tunapaswa kuwa wabunifu na kuhakikisha miradi yote tuliyonayo inafanya kazi. Stendi mpya mliyoizindua pamoja na mradi wa vibanda vilivyopo Manispaa ya Singida, hakikisheni ifikapo mwezi wa pili miradi hiyo iwe imekamilika na kuanza kufanya kazi.”

Katika ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo, Katibu Tawala huyo ametembelea miradi ya ujenzi wa shule za msingi Unyahati na Puma, ofisi ya Kijiji cha Issuna A, pamoja na Stendi ya Mabasi ya Ikungi.
Akiwa kwenye miradi ya shule za Puma na Unyahati, Dkt. Maganga aliagiza kuongezwa kwa mafundi wa ujenzi ili kuongeza kasi ya utekelezaji, na kuhakikisha miradi hiyo inakamilika ifikapo tarehe 10 Januari 2026, ikiwemo uwekaji wa madawati na shule kupata vibali vya kuanza kutumika rasmi.
Alisisitiza “Nahitaji kasi ya ujenzi iongezeke, mafundi wawe wengi. Ifikapo tarehe 10 Januari, miradi yote ya ujenzi wa shule iwe imekamilika kwa asilimia 100 na kwa ubora uliokusudiwa, ikiwemo madawati. Hakutakuwa na ongezeko lolote la fedha, hivyo simamieni miradi kwa umakini mkubwa.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa