Makamu wa Rais Mh. Samia Suluhu Hassan afanya ziara Wilayani Ikungi
Posted on: February 17th, 2019
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan amefanya ziara leo mapema tarehe 17/02/2019 Wilayani Ikungi na kufungua miradi ya Maendeleo. Mama Samia amezindua mradi wa maji utakaohudumia wakazi wananchi zaidi ya 2600 wa kijiji cha Ulyampiti kilichopo katika Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida.
Makamu wa Rais alitembelea zahanati ya Mang'onyi na kutoa agizo kwa Wizara ya Maji kuhakikisha katika mpango wa visima 20 wilayani Ikungi kimoja kichimbwe katika kijiji cha Mang’onyi. Pia Makamu alitembelea kituo cha Afya cha Ihanja na kujionea maboresho mbali mbali ikiwa pamoja na kufungwa mashine mpya ya upasuaji.
Akihutubia kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Ihanja Madukani Makamu wa Rais amesisitiza umuhimu wa Bima ya Afya kwa wananchi na kuzitaka mamlaka husika kutoa elimu ya kutosha ili kila mwananchi aelewe mpango wa Serikali wa Bima kwa wote.
Aidha Makamu wa Rais amewataka wakazi wa Ihanja kutoruhusu mimba za utotoni kwani zinawanyima fursa mabinti wao kuja kuwa viongozi na wataalam wa badae, pia aliwasihi wananchi kuacha kukeketa mabinti kwani ukeketaji una athari nyingi zikiwemo vifo wakati wa kujifungua. Makamu wa Rais amechangia mabati 200 kuunga mkono juhudi za Mbunge wa Jimbo la Singida Magharibi, Mhe. Elibariki Kingu ambaye amekabidhi leo mifuko ya saruji mia sita kwa ajili ya kusaidia kuendeleza maboma ya zahati na majengo ya shule. Pia Mbunge huyo amekabidhi chereni kumi kwa vikundi vidogo vidogo ili kuweza kujiendeleza kiuchumi na kuinua kipato chao. Aidha Makamu amesema kuwa Chama na Serikali ni kitu kimoja kwani wanashirikiana katika kila jambo la kuleta maendeleo kwa wananchi ambapo ilani ya uchaguzi imetekelezwa kwa kiwango kikubwa.