Wajasiriamali wa Ikungi wakabidhiwa vitambulisho vya biashara na Mkuu wa Wilaya
Posted on: January 9th, 2019
Wajasiriamali wenye mtaji usiozidi milioni 4 wamekabidhiwa vitambulisho vya biashara na Mheshimiwa Mkuu wa Wilaya Ndg, Miraji Mtaturu mapema leo Tarehe 08/01/2019. Vitambulisho hivyo vimegawiwa kwa wajasiriamali wa Wilaya ya Ikungi ikiwa ni kutekeleza agizo la Rais John Pombe Magufuli. Aidha sherehe hizo zilihudhuriwa na wajasiriamali wadogo wadogo, watendaji wa kata,Watumishi wa Halmashauri,Watumishi wa dini, Mwakilishi toka TRA Singinda, Mkuu wa kituo cha Polisi Ikungi na Mwanasheria.
Mkuu wa Wilaya alisisitiza kuwa wafanya biashara hao wanatakiwa kuwa waaminifu na kuvitunza vitambulisho hivyo ili visipotee. "Itakuwa kitu cha ajabu kama utagawa kitambulisho chako na kumpa mtu mwingine afanyie biashara, ikibainika kuwa hujawa mwaminifu basi kitambulisho kitanyang'anywa kwa kuwa utakuwa huna sifa ya kuwa na kitambulisho hicho".Alisema Mtaturu
Naye Mkurugenzi Mtendaji Ndg, Justice L. Kijazi aliwapongeza wafanya biashara hao kwa kutunukiwa vitambulisho hivyo na kuwasihi kuwa wavitumie vitambulisho hivyo kama maelekezo ya Serikali yanayosema. Pia alisisitiza kuwa wafanya biashara wadogo wajitokeze kwa wingi kuchukua vitambulisho hivyo. "Vitambulisho hivi haviuzwi isipokuwa gharama ya Shilingi elfu ishirini (20,000) ni kuchangia gharama ya kutengeneza vitambulisho hivyo. Mheshimiwa Rais John Pombe Magufuli anawajali sana wafanya biashara ndio maana ameamua kutoa vitambulisho hivyo ili mfanye kazi kwa uhuru bila kubuguziwa na mtu yeyote". Alisema Kijazi.
Nao wafanyabiashara walisema kuwa wamefurahishwa sana na hatua ya Serikali kwa kuwaona kwa jicho la karibu wafanyabiashara wenye mitaji midogo na kuipongeza sana Serikali ya Awamu ya tano
Pichani washiriki mbali mbali waliohudhuria Siku hiyo rasmi ya kugawiwa vitambulisho vya wafanyabiashara wadogo