Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Suleiman Jaffo amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ndg. Justice Kijazi kwa kutekeleza miradi mbalimbali ya Halmasauri kwa gharama ndogo sana ikilinganishwa na Halmashauri zingine
Kwa kutumia mfumo wa ‘force account’, wameweza kutumia kiasi cha sh. 420 milioni pekee kujenga ukumbi wa mikutano wa kisasa, na shilingi milioni 200 kujenga jengo kubwa la ofisi, huku akisisitiza na kuzitaka Halmashauri ambazo bado hazijaanza ujenzi wa majengo ya ofisi na kumbi za kisasa za mikutano kuja kujifunza Ikungi.
Waziri Jaffo akiwa kwenye ziara ya kawaida mkoani Singida, Akitokea Jijini Mwanza, alisema katika uongozi wake amepita kwenye halmashauri nyingi lakini hajawahi kukutana na jengo la ukumbi mzuri na wa kisasa kama huo wa halmahauri ya Ikungi.
“Mkurugenzi kilichonifurahisha ni namna mlivyozingatia thamani ya pesa(value for money) na ubora, nilisema nataka ofisi ya TAMISEMI ifanye mabadiliko na mapinduzi ya kiutendaji, tulikotoka huko nyuma hatukuwa na sifa nzuri, lakini leo hii kila mahali ukitazama ikiwemo hapa ikungi huwezi kuamini,” alisema
Alizitaka halmashauri za Kondoa na Iramba kwa kuanzia kuja kujifunza kupitia wenzao hao wa Ikungi, ambao idadi ya majengo yao yote yamegharimu sh 1.5 bilioni pekee “nataka wengine wakitaka kujenga ofisi waje kujifunza hapa, iwe duplicate kwa wengine kuja kucopy na kupaste,” alisema Jaffo
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Edward Mpogolo alisema kiasi hicho cha pesa sh 1.5 bilioni kilitolewa na Rais Magufuli kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa halmashauri hiyo kwenye eneo la utawala bora.
Alisema kati ya pesa hizo sh 1.3 milioni zimetumika kujenga ofisi, nyumba ya DC, na Hospitali ya wilaya, huku Serikali ikiwa tayari imewatengea fedha nyingine zaidi ya sh. milioni 500 kwa ajili ya kukamilisha mradi wa vituo vya afya vya Sepuka, Ihanji na Iyumbu.
Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ikungi Bw. Justice Kijazi, alisema tangu kuanzishwa kwa halmashauri hiyo mwaka 2013, watumishi wa eneo hilo wamekuwa wakipanga na kukodi majengo ya watu binafsi kwa mikutano mbalimbali, ikiwemo kutumia hadi nyumba za wageni kwa shughuli za ofisi.
Kijazi alisisitiza kuwa jengo la ukumbi huo mpya na wa kisasa mbali ya kutumika kwa shughuli mbalimbali za mikutano ya kikazi, lakini pia litatumika kama kitega uchumi cha kuingizia halmashauri hiyo mapato, huku Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Juma Ali Mwangi, akimuomba Waziri Jaffo kusaidia mchakato wa upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kujenga hospitali ya wilaya kwa ustawi wa afya ya wakazi wa eneo hilo.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa