Iyumbu, 28 Februari 2025 — Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Bw. Kastori Msigala, amewataka wataalamu wa ujenzi kuhakikisha matumizi sahihi ya fedha za serikali kwa kufuata taratibu na viwango vya kitaalamu kabla ya kuanza ujenzi wa miradi ya maendeleo.
Bw. Msigala alitoa wito huo leo wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika Kata ya Iyumbu, akiwa ameambatana na wataalamu mbalimbali kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Akiwa katika ziara hiyo, alitembelea Kituo cha Afya Iyumbu, Shule ya Sekondari Kingu, Ofisi ya Kata ya Iyumbu, pamoja na kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika baadhi ya maduka ya eneo hilo.
Kituo cha Afya Iyumbu kimetumia takribani shilingi milioni 500 na kinahudumia zaidi ya wananchi 32,650. Hata hivyo, Bw. Msigala alibaini baadhi ya majengo kupasuka baadhi ya Kuta kutokana na hali ya udongo wa mbuga.
Alisisitiza kuwa ni lazima wahandisi wa Halmashauri wafanye uchunguzi wa udongo (soil test) na uchunguzi wa vifaa vya ujenzi (material test) kabla ya kuanza ujenzi wowote wa majengo ya serikali ili kuhakikisha yanajengwa kwa ubora na kudumu kwa muda mrefu.
“Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Daktari Samia Suluhu Hassan, ameendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya miradi ya maendeleo. Ni jukumu letu kuhakikisha fedha hizi zinatumika kwa ufanisi na kuwafikia walengwa,” alisisitiza Bw. Msigala.
Katika ukaguzi wa maduka, Bw. Msigala alibaini kuwa baadhi ya wafanyabiashara wanaendesha shughuli zao bila kuwa na leseni. Aliagiza Afisa Biashara wa wilaya kuhakikisha anafanya ufuatiliaji wa wafanyabiashara wote wenye sifa ya kuwa na leseni, ili kuhakikisha wanapata na kulipa leseni zao kwa mujibu wa sheria.
“Ili maendeleo ya kweli yaweze kufikiwa, ni lazima mapato ya ndani yakusanywe kikamilifu. Mapato haya ndiyo yanayochangia kuboresha huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi,” aliongeza.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa