Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi imekopesha vikundi 11 mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 100 kupitia mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani.
Hafla ya utiaji saini wa mikataba ya mikopo iliyoambatana na mafunzo kwa vikundi vilivyopangiwa kupata mikopo hiyo imefanyika leo Septemba 30, 2025 katika ukumbi wa halmashauri.
Akizungumza katika hafla hiyo Mratibu wa Mikopo wilaya na Afisa Maendeleo jamii Makao Makuu, Bwana Emmanuel Mboje amesisitiza vikundi hivyo kutumia fedha hizi kwa malengo yaliyokusudiwa ili ziweze kuwanufaisha wanakikundi na jamii kwa ujumla.
Aidha, amewakumbusha kuzingatia masuala muhimu ikiwemo wajibu, haki na majukumu ya wanakikundi, utatuzi wa migogoro ya kikundi, usimamizi na uendeshaji wa miradi, utunzaji sahihi wa kumbukumbu za kifedha.
‘’Mikopo hii imetolewa kwa vikundi 10 vya wanawake na kimoja cha vijana katika Kata za Misughaa, Siuyu,Dung’unyi, Irisya, Kikio, Mtunduru na Puma’’ amesema Mboje.
Kwa upande wake Mwanasheria wa Wilaya, Bi. Lilian Kasanga amewapitisha wanufaika katika vipengele vya mkataba na kuwataka viongozi wa vikundi (Mwenyekiti, Katibu na Mwekahazina) kutimiza wajibu wao na kusimamia fedha hizo ziwasaidie ipasavyo.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa