Afisa Utumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Bi. Edna Palla, akimwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Ndugu Kastori Msigala, amewaagiza wakandarasi wote waliopata tenda za utekelezaji wa miradi ya ujenzi wilayani humo kuongeza idadi ya mafundi ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati, ifikapo tarehe 12 Januari, 2026.

Agizo hilo amelitoa wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo iliyofanyika tarehe 07 Januari, 2026 katika kata za Sepuka na Mgungira, ambapo amebaini uzembe wa baadhi ya mafundi pamoja na ucheleweshwaji wa vifaa vya ujenzi kwa baadhi ya wazabuni, hali inayosababisha miradi kuchelewa kukamilika kinyume na miongozo ya Serikali.
Katika ziara hiyo, Bi. Palla akiongozana na wakuu wa idara na vitengo, ametembelea mradi wa ujenzi wa madarasa mawili na matundu sita ya vyoo katika Shule ya Msingi Italala, mradi ambao upo hatua ya umaliziaji ambapo kwa upande wa vyoo umefikia hatua ya upauaji, na unatarajiwa kugharimu jumla ya shilingi milioni 59.6 hadi kukamilika.

Sambamba na hilo, timu hiyo ilitembelea mradi wa SWASH wa ujenzi wa matundu 19 ya vyoo katika Shule ya Msingi Mwau, ambapo ujenzi upo hatua ya uwekaji wa jamvi na kuanza unyanyuaji wa msingi, mradi unaotarajia kugharimu takribani shilingi milioni 47.2.

Aidha, katika Shule ya Msingi Mlandala pamoja na Zahanati ya Mlandala, timu ilikagua ujenzi wa madarasa mawili na matundu sita ya vyoo, ambapo mradi upo hatua ya upauaji. Kwa upande wa zahanati, miradi ya ujenzi wa kichomea taka, matundu matatu ya vyoo pamoja na mfumo wa maji ipo hatua za ukamilishaji na inatarajiwa kugharimu shilingi milioni 38.9.

Ziara hiyo pia ilihusisha ukaguzi wa mradi wa BOOST wa ujenzi wa madarasa mawili ya awali na matundu sita ya vyoo katika Shule ya Msingi Kaugeri, mradi unaotarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 12 Januari, 2026 na kugharimu shilingi milioni 64.
Mradi mwingine uliotembelewa ni ujenzi wa shule mpya ya msingi katika Kijiji cha Mwankalaja, unaotarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 125.2 kutoka kwenye mapato ya ndani ya Halmashauri, mradi huo upo hatua ya kutangaza zabuni kwa wazabuni ili kuanza utekelezaji mapema.
Ziara ya ukaguzi wa miradi ilihitimishwa katika Shule ya Msingi Ufana, kata ya Mgungira, ambapo timu ilikagua mradi wa BOOST wa ujenzi wa madarasa matatu na matundu sita ya vyoo unaogharimu shilingi milioni 82.6, na kwa sasa mradi upo hatua ya uchimbaji wa msingi.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa