Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yaendelea kuchukua hatua kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule za msingi kupitia ujenzi wa miradi ya BOOST Wilaya ya Ikungi.
Akifanya ziara hii leo Tarehe 25 Septemba, 2025 katika Wilaya ya Ikungi Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, akiambatana na timu ya ufuatiliaji pamoja na timu ya Menejimenti (CMT) Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, amepongeza Ikungi kupata miradi ya BOOST, usimamizi wa miradi na uagizaji wa vifaa vya ujenzi kwa bei nafuu kwa kuzingatia ubora hivyo kuwataka Wilaya za jirani kuiga taratibu hizo ili miradi iweze kukamilika haraka na kwa ubora Zaidi.
Dkt. Fatuma Mganga, ametembelea mradi huo wa ujenzi wa shule ya msingi mpya yenye mikondo miwili, Jengo la utawala pamoja na nyumba ya watumishi (2 in 1) Kijiji Cha Puma inayogharimu millioni 545.4 kupitia bajeti ya mwaka 2024/2025.
Akisoma taarifa ya ujenzi huo Mwalimu Wenseslaus Masire amesema kuwa baadhi ya faida za mradi huo ni pamoja na kupunguza changamoto ya msongamano uliokwepo katika shule ya msingi Puma yenye jumla ya wanafunzi 1315, walimu kuwa na wigo mpana kuwafikia wanafunzi wote pamoja na fursa ya wanafunzi kujifunza kwenye mazingira yakuvutia.
Ziara hiyo pia imetembelea na kukagua mradi wa uchimbaji wa kisima cha umwagiliaji chenye uwezo wa kumwagilia hadi ekari 40 kata ya Unyahati, pamoja na mradi wa ujenzi wa kituo kipya Cha afya Kata ya Migughaa unaogharimu milioni 250 na miradi yote ipo hatua za awali.
Katika ukaguzi huo, timu imependekeza kuongezwa kasi ya utekelezaji wa mradi ili ukamilike kwa wakati, sambamba na kuhakikisha ubora unaozingatia mahitaji muhimu yakiwemo vyoo rafiki kwa watoto wa kike, bustani na upandaji miti, miundombinu bora ya kunawia mikono, viwanja vya michezo na mifumo ya kuzimamoto. Pia wamependekeza kuandaliwa mazingira rafiki yatakayozuia usumbufu wa sauti za vyombo vya usafiri ili kudumisha utulivu wa wanafunzi darasani.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa