HALMASHAURI WILAYA IKUNGI YAPEWA KONGOLE KUPATA HATI SAFI MFULULIZO MIAKA 10
HALMASHAURI ya Wilaya Ikungi mkoani Singida imeng'ara ambapo katika kipindi cha mfululizo wa miaka 10 imepata hati safi kuanzia 2013/2014 hadi 2022/2023.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya, Justine Kijazi, amesema hayo leo Juni 25, 2024 wakati wa kikao maalum cha Baraza la Madiwani cha kujadili majibu ya hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Amesema kulingana na taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya kuishia Juni 2023,Halmashauri ilikuwa na hoja 5,hoja za miaka ya nyuma ni 24 na hoja za mwaka 2022/2023 ni hoja 28.
Kijazi amesema hoja 30 zilifungqa na kubaki na hoja 22 ambazo ziko kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji.
"Tunashukru sana ofisi ya Mkaguzi wa ndani ambayo ni jicho la halmashuri kusimamia hoja,sasa tunajiandaa na ukaguzi wa mwaka 2023/2024,tuendelee kuomba ushirikiano ili halmashuri iendelee kupata hati safi,tutaendelea kufanya kazi kwa kufuata sheria,kanuni,taratibu na miongozo ya serikali,"amesema Kijazi.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe.Halima Dendego, amesema ni jambo kubwa na la kupongezwa na kitia moyo kwa halmashuri kupata hati safi kwa mfululizo wa miaka 10.
Amesema wakaguzi wa ndani ni walimu wazuri sana ambao kama halmashuri inazingatia ushauri wao halmashuri haiwezi kuwa na hoja nyingi za ukaguzi.
"Katika Halmashauri ukiona hoja zinajitokeza ujue kuna mtu amekula bila kunawa, naagiza kila mzalisha hoja iwe ni idara abanwe," amesema Dendego.
Mkuu wa Mkoa ameagiza kuwa kudhibiti hoja mpya zisijitokeze katika mkutano wa kila mwezi wa Kamati ya fedha ajenda mojawapo iwe ni kujadili hoja za CAG kwani haiwezekani mtu anazalisha hoja halafu watu wanasumbuka kukutana na kuzijadili.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Mhe. Ally Mwanga amesema halmashuri hiyo kupata hati safi mfululizo kwa miaka 10 ni kutokana na ushirikiano uliopo wa watendaji na madiwani.
Akizungumza kuhusu hoja za CAG, amesema kimsingi hakuna halmashuri inayofurahia kuwa na wingi wa hoja hivyo jukumu la kila mmoja kuhakikisha hawazalishi hoja mpya.
"Hoja zilizopo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha zinajibiwa na sio kumuachia Mweka Hazina pekee yake," amesema Mwanga.
Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida,Dk.Fatuma Mganga, amesema kila halmashauri iweka mkakati madhubuti kujibu hoja za CAG ambapo kila halmashauri ziwe zaidi ya tisa.
Dk.Mganga amesema moja ya vigezo vya kupima utendaji wa halmashuri ni uwingi wa hoja hivyo kinachotakiwa ni kuongeza jitihada kuhakikisha hoja zilizopo zinajibiwa na kutozalisha nyingine.
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mhe.Thomas Apson amesema halmashuri hiyo inastahili pongezi kwa kupata hati safi mfululizo kwa miaka 10.
Aidha, Apson amesema halmashuri iongeze ubunifu kwa kuwa na vyanzo vipya vya mapato badala ya kila mwaka kuwa na vyanzo vile vile na kutolea mfano majimoto kwamba kinaweza kuwa chanzo kizuri cha mapato.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa