Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi leo tarehe 09 Juni, 2025 imefanya kikao maalumu cha Kamati ya Fedha, Uongozi na Mipango kwa ajili ya kujadili majibu ya hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2024.
Kwa mujibu wa taarifa ya ukaguzi wa hesabu za serikali kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2024, halmashauri ilikuwa na jumla ya hoja 40 kati ya hizo hoja za miaka ya nyuma ni 20 na hoja za mwaka wa fedha 2023/2024 ni 20 hadi sasa, halmashauri imefanikiwa kufunga hoja 9 za miaka ya nyuma na hoja 5 za mwaka wa fedha 2023/2024 hivyo kubakiwa na hoja 26 ambazo zipo katika hatua nzuri za utekelezaji.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Fatuma Mganga, Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Mheshimiwa Rashid M. Rashid, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Mheshimiwa Ally J. Mwanga, Waheshimiwa Madiwani; Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri, Ndugu Kastori Msigala, wakaguzi kutoka Ofisi ya Ukaguzi Mkoa, pamoja na wakuu wa idara na vitengo wa halmashauri.
Miongoni mwa masuala yaliyowekwa mezani ni pamoja na umuhimu wa kuchukua hatua za haraka ili kuondoa hoja au kupunguza idadi ya hoja, ili Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi iendelee kupata hati safi kwa miaka mfululizo.
PICHA NA MATUKIO
Kikao kilisisitiza kuwa hoja zinazoweza kufutwa ndani ya uwezo wa halmashauri ziondolewe mara moja, huku hoja zinazohitaji fedha zipewe kipaumbele katika vyanzo vya mapato ama ziwekwe kwenye bajeti ili kuweza kupunguza mzigo huo.
Mwenyekiti wa Halmashauri, Mheshimiwa Ally J. Mwanga, amesisitiza kuwa hoja ni kipimo cha utendaji wa halmashauri
“Wingi wa hoja si sifa, tunapaswa kuziondoa hoja zilizo ndani ya uwezo wetu na kwa zile zilizo nje ya uwezo, tujibidiishe kwa kila hali kuhakikisha tunazipunguza au kuziondoa kabisa ili halmashauri yetu iendelee kupata hati safi kila mwaka.”
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Fatuma Mganga, aliweka msisitizo kwa Halmashauri kuchukua hatua za haraka kufuta hoja hizo.
Kwa hoja ambazo ni za miaka ya nyuma na zinazohitaji fedha nyingi kufutika, Katibu Tawala alisisitiza kwamba Halmashauri iweke bajeti mahsusi kwa ajili ya kulipa madeni hayo.
“Kufuta hoja kunahitaji umakini na kujitolea, Mkurugenzi hakikisha hoja zinafutika,” alisisitiza.
Kwa kumalizia, Mheshimiwa Mganga aliwataka viongozi na watendaji kufanya kazi kwa ushirikiano (team work) ili kuongeza kasi ya ukusanyaji mapato.
“Kila mwaka mapato yanaongezeka, Nampongeza Mkurugenzi Msigala kwa kunihakikishia kuwa mwaka huu halmashauri itakusanya hadi shilingi bilioni 7, halmashauri isisahau kutenga asilimia 10 ya mapato hayo kwa ajili ya vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. kama mkataba wa Serikali unavyoelekeza. ” alisema.
Aidha, amehimiza kuwa majibu ya hoja yanapotolewa, yasiwe ya jumla jumla na yenye ushahidi ili kuweza kuwashawishi wakaguzi kufuta hoja husika.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa