Kata ya Ikungi, 31 Mei 2025 – Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ndugu Kastori Msigala, leo ameendelea na ziara yake ya kutembelea miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya hiyo.
Akiwa katika Kata ya Ikungi, Mkurugenzi huyo alitembelea zahanati ya Matongo, shule ya msingi na sekondari ya Matongo, shule ya msingi Dung’unyi pamoja na zahanati ya Ighuka.
Katika ziara yake kwenye zahanati ya Matongo, Ndugu Msigala alibaini kuwepo kwa changamoto mbalimbali katika matumizi ya Mfumo wa mapato wa Kielektroniki wa Serikali wa utoaji huduma za afya (GOTHOMIS). Mojawapo ya changamoto ni kutotumika ipasavyo kwa mfumo huo, ambapo baadhi ya dawa hazionekani kwenye orodha ya main store na sub store hivyo kutolingana na orodha ya bin card.
Alisema Hali hiyo, ikiwa haitadhibitiwa, inaweza kusababisha upotevu wa dawa na kuisababishia serikali hasara.
Ametoa maagizo dawa zote zinazonunuliwa kutoka Bohari ya Dawa (MSD) au kwa washitiri wengine, invoice na batch number za dawa zilingane na za kwenye mfumo huo. Pia ameagiza kuwa changamoto zote zinazohusiana na mfumo huo zitatuliwe haraka na mafunzo yatolewe kwa watumishi wote wasio na uelewa wa kutosha juu ya matumizi ya mfumo huo.
Katika zahanati ya Ighuka, Mkurugenzi Msigala ameagiza ukamilishaji wa ujenzi wa shimo la choo na sehemu zingine zilizobakia ukamilike haraka iwezekanavyo, kwani Serikali imeshatoa fedha kupitia mapato ya ndani kwa ajili ya kukamilisha mradi huo ili jamii inufaike.
Jumla ya shilingi milioni 12 tayari zimeingizwa kwenye akaunti ya zahanati hiyo kwa ajili ya umaliziaji wa ujenzi wa choo, shimo ,milango pamoja na sehemu zingine.
Aidha, Ndugu Msigala ameshauri uongozi wa zahanati hiyo kuwasiliana na kitengo cha manunuzi ili kufuata utaratibu wa kujaza imprest kupitia mfumo wa NEST, kwani taratibu zinaruhusu pale panapohitajika.
Kauli hiyo imetolewa kufuatia maelezo ya Mtendaji wa Kijiji cha Ighuka, Bi Monica Edward, aliyeeleza kuwa ucheleweshajwi wa umaliziaji wa mradi huo umetokana na mzabuni aliyepatikana kupitia mfumo wa NEST kuchelewesha vifaa vya ujenzi.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa