Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ndugu Kastori Msigala, ameendelea na ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo Ikungi , ambapo leo, Septemba 15, 2025, ilihusisha ukaguzi wa miradi ya ujenzi katika Kata ya Mang’onyi.
Akiwa ameambatana na Wakuu wa Divisheni, Msigala alitembelea miradi ya ujenzi katika Shule za Msingi Sambaru, Mbogho na Mwau, Shule ya Sekondari Mang’onyi Shanta pamoja na Zahanati ya Tupendane.
Katika ziara hiyo, aliwataka maafisa manunuzi kuhakikisha vifaa vya ujenzi vinapatikana kupitia mfumo wa ununuzi wa moja kwa moja kutoka viwandani (bulk purchase) ili kupunguza gharama.
Aidha, alimsisitiza afisa manunuzi wa wilaya kusimamia shughuli zote kwa kutumia mfumo wa NEST, hatua itakayorahisisha upatikanaji wa wazabuni kwa wakati na kuwasaidia walimu wanaopata changamoto mbalimbali ikiwemo kukosa wazabuni.
Msigala pia alisisitiza kuwa fedha zote za Mfuko wa Jimbo ziwekwe moja kwa moja kwenye akaunti husika za miradi badala ya kupitia akaunti za vijiji, ili kuimarisha uwajibikaji na usimamizi wa fedha za umma.
Ziara hiyo inalenga kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa miradi na kuhakikisha matumizi sahihi ya fedha za umma, ili wananchi wa Wilaya ya Ikungi wapate huduma bora za msingi, hususan katika sekta za elimu na afya.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa