Mafunzo kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya kata yamezinduliwa leo tarehe 4 AGOSTI 2025 katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Mafunzo hayo ya siku tatu yanawajumuisha washiriki 56 kutoka kata 28 za halmashauri hiyo.
Uzinduzi wa mafunzo hayo umehudhuriwa na viongozi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya jimbo na kata, maafisa TEHAMA, Afisa Uchaguzi, Afisa Manunuzi na watendaji mbalimbali wa Tume.
Akifungua rasmi mafunzo hayo, Msimamizi wa Uchaguzi wa Wilaya ya Ikungi, Bi. Edina Palla, aliwapongeza washiriki kwa kuchaguliwa kutekeleza jukumu hilo muhimu. Alisisitiza kuwa wanapaswa kufanya kazi kwa weledi wa hali ya juu ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa ufanisi na kwa mujibu wa sheria.
“Dhamana mliyopewa ya kusimamia na kuratibu uendeshaji wa uchaguzi wa Rais na Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania pamoja na Madiwani wa Tanzania Bara ni kubwa, nyeti na muhimu kwa mustakabali wa taifa letu,” alisema Bi. Palla.
Aliongeza kuwa ni muhimu kwa wasimamizi hao kuzingatia maadili ya kazi, uwajibikaji na weledi katika kipindi chote cha utumishi wao kwa Tume hadi kukamilika kwa uchaguzi mkuu.
“Vishirikisheni vyama vyote vya siasa vyenye usajili kamili katika hatua zote za uchaguzi kwa kuzingatia matakwa ya Katiba, Sheria, Kanuni na Maelekezo ya Tume,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Afisa Uchaguzi wa Wilaya ya Ikungi, Mwalimu Andrew Marwa, aliwataka washiriki kuwa makini katika mafunzo hayo na kuhakikisha wanayatumia ipasavyo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
“Mzingatie Katiba, Sheria, Miongozo na Maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume ili kuhakikisha zoezi la uchaguzi linafanyika kwa amani na mafanikio,” alisema Marwa.
Mafunzo hayo yanatarajiwa kuwajengea uwezo Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya kata katika kusimamia uchaguzi kwa uadilifu, weledi na kwa kuzingatia taratibu zote za kisheria
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa