Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Thomas Apson amesisitiza wamiliki wa magari ya abiria katika kijiji cha Makiungu kufuata utaratibu wa kupakia abiria Hospitali ya Makiungu na Stendi ya Makiungu kama alivyouweka wakati wa kusuluhisha mgogoro wa stendi mwaka Jana.Katika kikao kilichofanyika hii leo Tarehe 31, Januari, 2024, Mtendaji wa Kata ya Makiungu Bi-Nasra Abbas Mattaka amesema kuwa uongozi wa wamiliki wa magari, uongozi wa kijiji pamoja na uogozi wa kampuni ya mabasi ya Hope Express walikaa kujadili utaratibu ambao ulikuwa ukikiukwa na kampuni hiyo ambayo imekua ikipakia abiria kinyume na utaratibu uliowekwa hali ambayo inazua mgogoro baina ya wamiliki wa magari mengine."Hali hiyo imepelekea kuleta taharuki kwani tayari utaratibu ulishawekwa baada ya Mkuu wa Wilaya kufanya vikao kadhaa kati ya Uongozi wa Hospitali ya Makiungu na wamiliki wa vyombo vya abiria" Amesema Mtendaji wa kata hiyo.Kwa upande wake mmiliki wa magari ya Hope Express, Bwana Saidi amesema kinachofanya wakiuke utaratibu uliowekwa na Mkuu wa Wilaya kwa sababu ya ratiba walizopewa na LATRA hali inayowalazimu kupakia abiria mapema ili waondoke kwa muda kuelekea Igunga."Hivyo tunaomba kupakia abiria katika Hospitali ya Makiungu kwa muda wa saa moja kuanzia saa 7 hadi saa 8 kwani hospitali ndipo wanapopatikana abiria wengi zaidi ya stendi", amezungumza Bwana Saidi.Baadhi ya madereva na wamiliki wa magari wamesema hawana tatizo na kampuni hiyo mpya inayofanya safari zake kutoka Igunga mpaka Makiungu. Madereva wamesema cha msingi Hope Express wafate utaratibu ambao wameukuta kwani ni utaratibu ambao hauleti migogoro kama ilivyo sasa.Mwisho, Mkuu wa Wilaya amemaliza na kusema kuwa utaratibu aliouweka kwa makubaliano ya pande zote ufuatwe kama ulivyo kwani ndio njia pekee yakuepukana na migogoro."Cha msingi, uongozi wa kampuni ya Hope Express ukae na uongozi wa magari ya abiria kata ya Makiungu ili wapewe zamu na kufuata utaratibu na sio kila gari mpya inayokuja ifuate utaratibu wake wenyewe", amesema Mkuu wa Wilaya ya Ikungi.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa