DC MTATURU ATOA ONYO KWA WAHAMASISHAJI WA MAANDAMANO
Posted on: March 15th, 2018
Kwa hisani ya Mathias Canal,
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida Mhe Miraji Mtaturu ametoa onyo kwa wanaohamasisha kufanyika kwa maandamano katika wilaya hiyo kuacha mara moja vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kufuatia hilo amewaasa wananchi kutokubali kurubuniwa na watu hao na badala yake wajikite katika shughuli zitakazowaingizia kipato.
Mtaturu amesema kumekuwa na minong`ono ya uwepo wa maandamano jambo ambalo anawaasa waachane nalo.
“Nimesikia dalili kwamba kutakuwa na maandamano,nawaomba wananchi waachane na hayo mambo ambayo hayana msingi kwao,hao wanaotaka kuandamana hawana kazi za kufanya,
“Sisi tuna kazi za kufanya tusiingie kwenye mkumbo wa kushiriki katika jambo ambalo litatuathiri sisi na familia zetu hivyo tusipoteze muda twendeni tukafanye kazi,mtu anayekuhamasisha jambo ambalo halina manufaa na wewe achana nae muda wa kufanya siasa haupo sasa hivi kila mmoja afanye shughuli zake,”