Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ndg. Kastori Msigala, amekutana na watendaji wa kata na vijiji kwa lengo la kufahamiana nao na kuweka mikakati ya pamoja ya utendaji kazi.
Akizungumza katika kikao hicho, Ndg. Msigala amesema kuwa tangu alipoteuliwa Januari 2025, hajaweza kukutana rasmi na watendaji hao, hivyo kikao hicho kilikuwa fursa ya kufahamiana na kubadilishana mawazo juu ya namna bora ya kutekeleza majukumu.
"Watendaji wa kata na vijiji mnapaswa kunipatia taarifa zote za maeneo yenu ya kazi, ikiwemo changamoto zinazowakabili ninyi pamoja na wananchi ili hatua za haraka zichukuliwe katika kuzitatua," ameeleza Ndg. Msigala.
Akiweka bayana mfumo wake wa kazi, Msigala amesema utakuwa akikaa ofisini kwa ajili ya kushughulikia taarifa mbalimbali kutoka kwa wakuu wa idara na vitengo, pamoja na kusaini nyaraka muhimu, sambamba na kutoka nje ya ofisi kwa ziara za ukaguzi wa miradi ya maendeleo na ukusanyaji wa mapato.
"Ninataka mnijue ninahitaji nini, sitaki uongo wala visingizio, ninataka vitendo,fanyeni kazi kwa weledi kuhakikisha mnatatua kero za wananchi katika maeneo yenu," amesisitiza.
Aidha, Mkurugenzi Msigala amekemea vikali tabia ya baadhi ya watendaji kuingia mikataba isiyo halali, akibainisha kuwa mikataba yote ya halmashauri ni lazima iandaliwe na mwanasheria wa halmashauri na kusainiwa na Mkurugenzi Mtendaji pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri.
Kwa lengo la kuongeza hari ya ukusanyaji mapato, amesema Halmashauri imepanga kutoa motisha kwa watendaji wa kata na vijiji mpaka asilimia 10 ya mapato waliyokusanya , ili waweze kufidia gharama mbalimbali za ukusanyaji mapato kama vile posho za kuwalipa migambo wanaokaa magetini, nauli, na gharama nyingine zinazojitokeza.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa