Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi Aprili 10, 2019 amezindua rasmi huduma za Afya za CHF iliyoboreshwa katika mkoa wa Singida ambapo amewataka wananchi wa mkoa wa Singida kujitokeza kwa wingi ili kujisajili katika huduma za BIMA na CHF iliyoboreshwa ili kuwa na uhakika wa tiba kwa familia zao kwa mwaka mzima ndani ya mkoa katika hospitali zote zilizounganishwa na mfumo wa CHF uliyoboreshwa.
Dkt. Nchimbi akizungumza na wananchi hao amesema, kutokujali na kuzingatia afya, na kufanya makusudi ya kutokujihusisha na miundombinu na mifumo ambayo imeelekezwa na kuandaliwa na Serikali ya kumsaidia kila mwananchi kuwa na uhakika wa afya bora ni kosa la kijinai.
“Tunasisitiza kwamba kila mkazi wa mkoa wa Singida, ahakikishe anajiunga na mfuko huu ili kuwa na uhakika wa kupata matibabu hata wakati hana fedha”
“Kuna watu wenye fikra potofu eti hawawezi kujiunga na bima ya afya kabla ya kuugua. Huo ni uchuro mkubwa”.
“Ugonjwa hauna tabia ya kutoa taarifa kuwa tarehe fulani utamkumba mtu fulani. Unakuja ghafla bila matarajio ya mhusika. Mhusika anakuwa hana hela wala mjomba wa kumsaidia, hii ni hatari kwa usalama wa mtu huyo”. amesema Dkt. Nchimbi Aidha, Mkuu huyo wa mkoa wa Singida, amewahimiza wananchi hao kufanya kazi kwa bidii na maarifa ili kuepusha miili yao kuwa nyumba ya milolongo ya magonjwa mbalimbali yasiyoisha.
Amesema, binadamu mwenye nguvu ya kufanya kazi na akawa hafanyi kazi, mwili wa mtu huyo hudhoofika kwa kasi na kuruhusu kirahisi magonjwa ya kila aina kumuingia.
“Wavivu wa aina hii wanaoruhusu kwa makusudi maradhi kuwaingia, BIMA iliyoboreshwa sio rafiki yao. Kufanya kazi kwa bidii ni kinga tosha ya mwili. Asiyefanya kazi kwa bidii huyo anaruhusu magonjwa kumwingia kirahisi”, Dkt. Nchimbi
Akifafanua zaidi kuhusu bima ya afya iliyoboreshwa amesema, ni kinga tosha inayomlinda mwanachama na familia yake ya mke/mme mmoja na watoto wanne walio na umri wa chini ya miaka 18.
Kwa upande wake mwakilishi wa Meneja wa CHF Taifa, Slivery Mgonza, amesema bima hiyo imeboreshwa pamoja na mambo mengine, imepanua maeneo ya kutoa huduma. Kwa sasa mwanachama atakuwa na fursa ya kutibiwa sehemu yoyote ndani ya mkoa tofauti na zamani.
Amesema, usajili wake kwa sasa umekuwa rahisi, mambo ya kalete picha sasa hayapo. Kila kitu kinapatikana kwenye vituo vya usajili.
Naye, Mganga mkuu wa mkoa wa Singida, Dkt. Victoria Ludovick amesema kuanzia Januari hadi Desemba mwaka 2018, idadi ya walengwa wa CHF walitambuliwa, kati yao 54,569 walifanikiwa kujiunga na mfuko wa bima ya afya ya jamii.
Akisisitiza zaidi amesema, jumla ya shilingi 502,825,000, za mfuko wa CHF zilikuwasanywa kutoka halmashauri zote saba. Fedha za tele kwa tele zilizoombwa na halmashauri zote ni shilingi 347,889,000. Kati ya hizo, shilingi 20,330,000 tu, zililipwa kwa halmashauri ya Ikungi.
Wakati huo huo, fundi ujenzi manispaa ya Singida, Hassan Ikingu ambaye alijiunga na mfuko huo jana, amesema mfuko huo wa bima pamoja na faida zake nyingi, unasaidia mno kupunguza gharama kubwa za sasa za matibabu.
“Sasa hivi kwa sisi wananchi wenye kipato cha chini, si rahisi kumudu gharama za matibabu zinazotozwa na vituo vya kutolea huduma za afya. lakini ukiwa na bima ya afya ya jamii, hata kama huna fedha unauhakika wa kupata matibabu ya gharama yoyote”, amesema Ikingu.
MATUKIO KATIKA PICHA
Huduma za usajili wa BIMA iliyoboreshwa zikiendelea kutolewa kwa wananchi katika uwanja wa zamani wa stand ya mabasi katika Manispaa ya Singida, wakati wa kilele cha uzinduzi wa mfuko wa bima ya afya ya jamii (CHF) ulioboreshwa, mkoani Singida.
Kikundi cha ngoma cha mbalamwezi kikitoa burudani wakati wa kilele cha uzinduzi wa mfuko wa bima ya afya ya jamii (CHF) ulioboreshwa, mkoani Singida.
Mganga mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Victoria Ludovick akizungumza wakati wa kilele cha uzinduzi wa mfuko wa bima ya afya ya jamii (CHF) ulioboreshwa, mkoani Singida.
Mwakilishi wa Meneja wa CHF Taifa, Slivery Mgonza, akizungumza wakati wa kilele cha uzinduzi wa mfuko wa bima ya afya ya jamii (CHF) ulioboreshwa, mkoani Singida.
Katibu Tawala mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi akizungumza wakati wa kilele cha uzinduzi wa mfuko wa bima ya afya ya jamii (CHF) ulioboreshwa, mkoani Singida.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi (mwenye kisemeo) akihamasisha zoezi la uchangiaji wa huduma za CHF iliyoboreshwa kwa ajili ya kuwapatia wananchi wasio na uwezo wa kuchangia, wakati wa kilele cha uzinduzi wa mfuko wa bima ya afya ya jamii (CHF) ulioboreshwa, mkoani Singida.
Katibu Tawala mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi (wa pili kulia) akichangia huduma ya CHF iliyoboreshwa kwa ajili ya mwananchi mmoja (aliyebeba mtoto) ili aweze kupatiwa kadi ya huduma ya afya ya CHF iliyoboreshwa, wakati wa kilele cha uzinduzi wa mfuko wa bima ya afya ya jamii (CHF) ulioboreshwa, mkoani Singida.
Mganga mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Victoria Ludovick akichangia huduma ya CHF iliyoboreshwa kwa ajili ya mwananchi mmoja (mama mjane, wa kwanza kulia) ili aweze kupatiwa kadi ya huduma ya afya ya CHF iliyoboreshwa, wakati wa kilele cha uzinduzi wa mfuko wa bima ya afya ya jamii (CHF) ulioboreshwa, mkoani Singida.
Mwakilishi wa shirika la World Vision mkoani Singida akipongezwa mara baada ya kuchangia kaya kadhaa za halmashauri mbalimbali za mkoa wa Singida ili aweze kupatiwa kadi ya huduma ya afya ya CHF iliyoboreshwa, wakati wa kilele cha uzinduzi wa mfuko wa bima ya afya ya jamii (CHF) ulioboreshwa, mkoani Singida.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza, wakati wa kilele cha uzinduzi wa mfuko wa bima ya afya ya jamii (CHF) ulioboreshwa, mkoani Singida.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi mara baada ya kubonyeza king'ola cha uzinduzi rasmi wa CHF iliyoboreshwa mkoani Singida wakati wa kilele cha uzinduzi wa mfuko wa bima ya afya ya jamii (CHF) ulioboreshwa, mkoani Singida.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akikabidhi kadi za huduma ya afya za CHF iliyoboreshwa, wakati wa kilele cha uzinduzi wa mfuko wa bima ya afya ya jamii (CHF) ulioboreshwa, mkoani Singida.
Mkuu wa mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akiwa katika picha ya pamoja na watoto pamoja na mwakilishi wa wazazi waliopatiwa kadi za huduma za CHF iliyoboreshwa, wakati wa kilele cha uzinduzi wa mfuko wa bima ya afya ya jamii (CHF) ulioboreshwa, mkoani Singida.
Sehemu ya wananchi mbalimbali waliojitokeza kushuhudia kilele cha uzinduzi wa mfuko wa bima ya afya ya jamii (CHF) ulioboreshwa, mkoani Singida.
Sehemu ya meza kuu
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa