Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ussi, amekagua na kuridhishwa na utekelezaji wa Mradi wa Ujenzi wa Shule Mpya ya Sekondari ya Amali ya Samamba iliyopo katika Kijiji cha Utaho ‘A’, Kata ya Kintuntu.
Mradi huo ulianza kutekelezwa tarehe 15 Oktoba 2024 baada ya Halmashauri kupokea fedha tarehe 30 Juni 2024, na kufanikisha ujenzi wa majengo muhimu ikiwa ni pamoja na vyumba vya madarasa 8, maabara 2, jengo la utawala, chumba cha TEHAMA, maktaba, tanki la maji, vyoo na nyumba ya mwalimu. Ufundishaji ulianza rasmi tarehe 17 Machi 2025 baada ya shule kusajiliwa kwa namba S.6861.
Gharama ya mradi imefikia shilingi 609,605,626 ambapo Serikali Kuu kupitia mpango wa SEQUIP ilichangia shilingi 544,225,626, Halmashauri shilingi 32,450,000, wananchi ekari 25.8 zenye thamani ya shilingi 12,930,000, huku wahisani wakichangia shilingi 20,000,000 kwa uchimbaji wa kisima cha maji.
Shule hiyo ambayo kwa sasa ina walimu 10 na wanafunzi 81 wa kidato cha kwanza, inalenga kutoa elimu bora ya karibu na kuongeza fursa za kujiajiri kwa vijana kupitia masomo ya amali. Vilevile, mradi umetoa ajira kwa walimu na jamii inayozunguka shule hiyo.
Mwenge wa Uhuru umepongeza juhudi za Serikali, Halmashauri, wananchi na wadau kwa kushirikiana kuboresha mazingira ya elimu, huku matarajio yakiwa ni kuwapatia wanafunzi na walimu mazingira bora ya kujifunzia na kufundishia.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa