Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Halima Dendego akiongozana na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt Fatuma Mganga ameagiza kufungwa kwa hoja 19 zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika Wilaya ya Ikungi ifikapo Julai mwaka huu.
Akizungumza leo Juni 17, 2025 katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi cha kujadili majibu ya hoja zilizoibuliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) amesema kuwa adhima ya Mkoa wa Singida ni kupunguza kwa kiasi kikubwa hoja za ukaguzi na hatimaye kuzimaliza kabisa ili kutengeneza sifa nzuri na mfano wa kuigwa kwa mikoa mingine.
Hata hivyo ameipongeza Wilaya ya Ikungi kwa kutokuwa na hati chafu kwa miaka 10 ya fedha mfululizo kuanzia mwaka wa fedha 2013/2014 hadi kufikia mwaka wa fedha 2023/2024 na yote yaliyoagizwa yaendelee kutekelezwa ili ifikapo tarehe 15 Julai 2025 kusiwe na hoja.
“Nikupongeze sana Mkurugezni Mtendaji Ndg. Kastori Msigala kwa juhudi zako kwani tangu umekuja nayaona mabadiliko mkubwa hasa upande wa mapato namba zinabadilika” alipongeza Dendego
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mheshimiwa Thomas Apson amesema kuwa kuna uwezekano mkubwa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi kukusanya bilioni saba kutokana na mikakati iliyopo ya kuziba mianya ya upotevu wa mapato.
“Tulikuwa tukifanya vizuri zaidi kwenye upande wa uvuvi na kwasasa tunaahidi kufanya vizuri pia kwenye upande wa ukusanyaji wa mapata kupitia mazao” amezungumza Apson
Akifunga baraza hilo Mheshimiwa Ally J. Mwanga amesema kuwa kwa kushirikiana kwa karibu na Halmashauri watahakikisha hoja 19 zilizosalia ziweze kufungwa pia amesisitiza kutokuzalishwa kwa hoja zisizo za msingi ili kuondoa sifa mbaya kwa Halmashauri.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa