JUMUIYA ya watu wanaoishi nje ya wilaya ya Ikungi,Mkoani Singida wamesajili taasisi ya kuibua na kuendeleza vipaji vya michezo kwa vijana kwa ajira endelevu ijulikanayo kwa jina la Ikungi Singida Sports Promosion (ISSP) itakayohakikisha michezo katika Halmashauri ya wilaya ya Ikungi inanyanyuka sambamba na vijana kupata ajira kupitia michezo hiyo.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Ikungi Singida Sports Promosion ,Salvatory Alute aliyasema hayo kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi wakati wa hafla ya kuitambulisha taasisi hiyo wilayani Ikungi na kukabidhi msaada wa mipira kwa baadhi ya shule za msingi na sekondari zilizopo katika Halmashauri hiyo.
Mwenyekiti huyo hata hivyo alifafanua kwamba lengo la kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kuhakikisha kwamba michezo katika Halmashauri hiyo,katika Mkoa wa Singida na baadaye katika nchi nzima inanyanyuka na watoto wanapata ajira,watoto wanarudisha nyumbani kile wanachokipata,uchumi unakuwa katika eneo hilo huku wazazi na jamii kwa ujumla inafaidika.
Aidha Mwenyekiti Alute aliweka bayana kuwa kwa hivi sasa wamebaini kwamba kuna baadhi ya watoto wenye vipaji vya michezo lakini wanaishia kwenye ngazi za chini hawaonekani na hawaonekani kwa sababu hakuna mtu wa kuwasaidia.
“Lakini nishukuru pia kwamba mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi ametupokea vizuri na ameahidi kushirikiana na sisi kwa sababu taasisi kama taasisi haiwezi kuanzisha kitu kipya ila tutaingia katika mifumo ya kiserikali iliyopo kwa mfano mashuleni tutakuwa na kalenda ya shule tutakuwa tunasaidia pale ambapo kalenda ya michezo itakavyokuwa inaonyesha”aliweka bayana mwenyekiti huyo.
Kwa mujibu wa Alute ambaye pia ni Afisa elimu msingi katika Halmashauri ya wilaya ya Arusha kwa sasa hivi wanakwenda kwenye michezo ya Umisseta na Umitashimta kwa hiyo wao kama taasisi watajikita katika kuhakikisha kwamba michezo hiyo inakwenda vizuri kuanzia ngazi ya maandalizi na ushiriki wa watoto unakuwa mpana zaidi.
Kwa upande wake Afisa elimu msingi wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi,Marhareth Kennan Kapolesya alisema kwamba kwa uwezo wake Mungu Halmashauri hiyo ina watu wenye vipaji sana vya kukimbia kwani vitu kama hivyo siyo kama vinapatikana kwenye kila sehemu ,bali hiyo ni zawadi kutoka kwake kwani mungu hutoa zawadi tofauti tofaui kwa kila sehemu.
Akitoa mfano ofisa huyo mwenye dhamana ya kusimamia sekta ya elimu alibainisha kuwa kwa kipindi cha miaka miwili mfululizo kwa ngazi ya Mkoa kwenye Umitashimuta Halmashauri hiyo kimkoa imechukua ushindi wa ujumla kwa nyanja zote wapo sawa,lakini kwa kombe la riadha hilo hawana shaka ya wao kulinyakua kwakila mwaka.
Mkuu wa shule msaidizi shule ya sekondari Unyahati,Jofrey Daudi Mianga alijigamba kwamba mwaka uliopita kuna vijana kutoka katika shule hiyo walishiriki michezo ya mbio za marathoni na baadhi yao walienda kushiriki mpaka ngazi ya taifa na kushika nafasi ya pili na kuongeza
kuwa kutokana na uwepo wa taasisi hiyo wanaweza kuhamasika zaidi na kuongeza jitihada kwenye sekta ya michezo.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa