Katibu Tawala Wilaya ya Ikungi Mhe.Rashid M.Rashid akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Thomas Apson amezindua rasmi kampeni ya kitaifa ya chanjo ya mifugo katika kijiji cha Mungaa kilichopo jimbo la Ikungi mashariki leo tarehe 08Julai, 2025.
Akizungumza na wananchi wa Mungaa amesama kuwa Kampeni hii ni sehemu ya mpango wa miaka mitano wa Serikali ya awamu ya Sita unaolenga kudhibiti magonjwa ya mifugo na kuongeza uzalishaji wa mazao ya mifugo nchini.
Kampeni hii imeanzishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na inafadhiliwa kwa ruzuku ya serikali yenye thamani ya Shilingi bilioni 216, ambapo mifugo inachanjwa kwa gharama nafuu ili kufikia soko la kimataifa, lengo kuu ni kuhakikisha angalau asilimia 70 ya mifugo nchini inapata chanjo
DAS ameeleza kuwa Wilaya ya Ikungi ina zaidi ya ng’ombe 418,000, mbuzi 222,000, kondoo 79,000 na kuku zaidi ya 900,000 hivyo wilaya imepokea chanjo zaidi ya milioni moja kwa ajili ya kuku, ng’ombe, mbuzi na kondoo, pamoja na hereni za kielektroniki kwa ajili ya utambuzi wa mifugo kwa huyo.
"Nawasisitiza wafugaji wote muwe mstari wa mbele kuwapa mifugo yenu chanjo hizi ili kuweza kupata mifugo inayokizi soko la kimataifa" amezungumza DAS
Mheshimiwa Rashid ametaja bei elekezi ya chanjo ya homa ya mapafu kwa ng’ombe inatolewa kwa Shilingi 500, kwa mbuzi na kondoo ni Shilingi 300, huku chanjo kwa kuku ikiwa bure, aidha viongozi wa vijiji na vyama vya wafugaji wametakiwa kushirikiana kuhakikisha wafugaji wanapeleka mifugo yao katika vituo vya chanjo.
Mwisho ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kuchanja mifugo yao, na kufuata hatua nyingine za kinga kama kuogesha mifugo, kutoa tiba sahihi na kufuata karantini pale mlipuko unapotokea.
Kwa upande wake Afisa Kilimo Wilaya ya Ikungi Ndg. Issa Mtweve amesema anaishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kuleta mpango wa chanjo ya rukuzu na kuwataka wafugaji kutumia fursa hiyo kwa kujitokeza kuchanja mifugo yao.
"Kampeni hiyo itaendelea katika vijiji vyote vya wilaya ya Ikungi kuhakikisha elimu inatolewa na mifugo yote inapata chanjo kwa muda elekezi" ameongeza Mtweve
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa