Mwenyekiti wa Baraza la Wafanyakazi Ndg. Justice L. Kijazi ameendesha Kikao hicho leo tarehe 18/09/2018 kilichofanyika katika Ukumbi wa Sekondari ya Ikungi. Kikao hicho kimehudhuriwa na wawakilishi wa vyama vya wafanyakazi, viongozi wa kamati tendaji ya Baraza na wajumbe mbalimbali wakiwemo wakuu wa idara na vitengo. Kikao hicho kimejadili stahiki za wafanyakazi, nidhamu na uadilifu katika utendaji kazi. Halmashauri imeweza kulipa madeni ya watumishi Jumla ya Tsh. 106,619,300 zikiwemo fedha za kujikimu kwa watumishi wanaoanza kazi.
"Tutajitahidi kama si kumaliza basi kupunguza madeni ya watumishi kwa kadri tutakavyoweza na hatutaweza kumhamisha mtumishi yeyote kabla ya fedha kutengwa kwa ajili ya kumlipa mtumishi anayehama." Alisema Kijazi
Aidha wajumbe wameipongeza Halmashauri kwa kupandisha watumishi madaraja kwa mwaka wa fedha 2015/2016 kwa asilimia 99. Pia wajumbe wameomba Halmashauri iwapandishe madaraja watumishi wanaotakiwa kupanda madaraja mara kibali cha kupandisha kitakapotelewa kwani kilisitishwa ili kupisha uhakiki wa vyeti vya Taaluma vya wafanyakazi.
"Tunaomba walimu wenye ulemavu wapewe vitendea kazi na kuangaliwa kwa jicho la karibu" Alisema mjumbe wa wawakilishi wa walimu wenye ulemavu. Mwenyekiti alipokea maombi hayo na kuahidi kuwa ofisi yake itabeba hitaji hilo na kulifanyia kazi haraka iwezekanavyo ikiwemo kununua karatasi maalumu za kuandalia masomo kwa walimu wenye ulemavu na kuahidi kuwa ofisi yake itatenga siku maalumu na kuwatembelea walimu wenye ulemavu ili kujua changamoto zinazowakabili.
"Hatutawavumilia viongozi wenye tabia ya kuwanyanyasa watumishi walio chini yao na itakapobainika hatua kali zitachukuliwa dhidi ya viongozi wenye tabia hiyo". Alisema Mwenyekiti kwa hisia kali.
Vile vile alisisitiza kuwa viongozi wakasimamie nidhamu na uwajibikaji kazini na kuwaasa kuachana na mambo yatakayowaingiza kwenye migogoro