Mafunzo kwa waandishi wasaidizi na waendesha mashine za BVR (Biometric Voter Registration) yamefunguliwa rasmi leo 14, May 2025, katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida. Mafunzo hayo ni sehemu ya maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura – Awamu ya Pili, unaotarajiwa kufanyika tarehe 16 hadi 22 ,Mei 2025.
Akifungua rasmi mafunzo hayo, Afisa Mwandikishaji wa Wilaya ya Ikungi, Dkt. Anthony Mwangolombe, aliwataka washiriki kuyazingatia mafunzo kwa makini ili waweze kutekeleza jukumu hilo la kitaifa kwa weledi, ujuzi na uadilifu wa hali ya juu.
“Ninawasihi mzingatie mafunzo haya kwa umakini. Zoezi hili linahitaji umahiri, nidhamu na uaminifu mkubwa kwa kuwa ni sehemu ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025,” alisema Dkt. Mwangolombe.
Mafunzo hayo yamekwenda sambamba na uwekaji wazi wa Daftari la Awali la Wapiga Kura, ambapo majina ya wapiga kura yamebandikwa katika vituo walivyojiandikishia, ikiwa ni hatua muhimu kuelekea uandikishaji rasmi.
Washiriki wa mafunzo hayo wanajumuisha waandishi wasaidizi, waendesha BVR, maafisa wasaidizi waandikishaji wa majimbo na kata, pamoja na wakufunzi kutoka Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Zoezi rasmi la uandikishaji wapiga kura wapya na uboreshaji wa taarifa litafanyika kuanzia tarehe 16 hadi 22 Mei, 2025, katika kata zote za majimbo ya Ikungi Mashariki na Ikungi Magharibi. Jumla ya vituo 72 vya uandikishaji vitatumika katika kipindi hicho.
Dkt. Mwangolombe alibainisha kuwa:
“Uboreshaji huo utahusisha kuandikisha wapiga kura wapya ambao ni raia wa Tanzania wenye umri wa miaka 18 na zaidi, au watakaotimiza umri huo kufikia siku ya uchaguzi mkuu mwaka 2025. Pia, wapiga kura waliopoteza au kuharibu kadi zao watapewa kadi mpya, na wale walioandikishwa awali watapewa fursa ya kurekebisha taarifa zao, zikiwemo majina na taarifa nyingine muhimu.”
Aidha, aliongeza kuwa mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya uandikishaji wakati wa uboreshaji wa daftari hilo, ili kusaidia kuimarisha uwazi na kuwasaidia kutambua waombaji wa maeneo husika.
“Tume imetoa vibali kwa jumla ya asasi za kiraia 157 kutoa elimu ya mpiga kura wakati wa uboreshaji wa daftari. Ni muhimu wadau wote kushirikiana na asasi hizo ili kufanikisha zoezi hili,” alisisitiza.
Vilevile, alieleza kuwa taarifa za wapiga kura waliohama kutoka kata au majimbo waliyosajiliwa awali zitahamishwa, na taarifa za wale waliopoteza sifa za kuwamo kwenye daftari – kama waliofariki dunia – zitaondolewa.
Mwisho wa hotuba yake, Dkt. Mwangolombe aliwatakia washiriki mafunzo mema na kuhitimisha kwa kusema:
“Ninawatakia mafunzo mema na utekelezaji mzuri wa jukumu hili muhimu lililo mbele yenu. Na sasa, natamka rasmi kuwa mafunzo haya yamefunguliwa.”
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa