Katibu Tawala wa Wilaya ya Ikungi, Mhe. Rashid M. Rashid, akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mhe. Thomas Apson, ameishukuru Serikali ya Korea kupitia ubalozi wake nchini Tanzania kwa kufanikisha mradi wa kuwawezesha wanawake na wasichana kiuchumi ili kufikia usawa wa kijinsia.
Akizungumza katika kikao kilichofanyika Septemba 17, 2025, cha kutoa taarifa kwa wadau kuhusu mradi uliofadhiliwa na Serikali ya Korea kupitia KOICA na kutekelezwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa (UN Women na UNFPA) kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Mhe. Rashid alisema mradi huo umeleta matumaini mapya kwa jamii.
“Tumeshuhudia wanawake wakijitokeza kwa ujasiri kuchukua nafasi katika shughuli za uzalishaji, uongozi wa vikundi, na hata kushiriki maamuzi ya kijamii. Wasichana nao wamepata ujuzi wa kujitegemea na kutambua thamani yao katika jamii,” amesema Mhe. Rashid.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ndugu Kastori Msigala, amesema matokeo chanya ya mradi wa pamoja wa KOICA–UN Women yanaendelea kuonekana kupitia ufadhili wa wilaya, umiliki wa jamii, na uongozi wa wanawake.
“Zaidi ya yote, Wilaya ya Ikungi inajivunia kusimama kama mfano wa kuigwa katika kuendeleza uwezeshaji wa kiuchumi wa wanawake na mipango ya usawa wa kijinsia hapa nchini Tanzania,” amesema Msigala.
Katika kikao hicho, wadau wametoa mafunzo kwa wanufaika wa mradi yaliyolenga kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu za kupinga dhidi ya ukatili wa kijinsia pia wametoa msaada wa kompyuta mbili, mashine ya fotokopi na meza.
Mafanikio yaliyopatikana kupitia utekelezaji wa mradi huo ni pamoja na ununuzi wa gari kwa ajili ya ufuatiliaji wa shughuli za uwezeshaji wa wanawake kiuchumi na kupinga ukatili wa kijinsia, matumizi ya kituo cha Huduma kwa pamoja (One stop centres) na Dawati la Jinsia yanayotoa msaada wa haraka na wa kitaalamu kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia, umilikishaji wa ardhi kwa wanawake, pamoja na ujenzi wa soko la kisasa Ikungi, linalotoa fursa kwa wanawake na wakulima kuuza mazao yao katika mazingira salama, safi na yenye hadhi.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa