Ikungi, 24 Februari 2025 – Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ndugu Kastori Msigala, akiambatana na wataalam wa halmashauri, ametembelea miradi ya ujenzi wa madarasa na mashimo ya vyoo katika shule za msingi Samaka, Dadu, Kintandaa, na Mnang’ana.
Ziara hiyo ni muendelezo wa juhudi za mkurugenzi huyo katika kufuatilia utekelezaji wa miradi mbalimbali inayoendelea ndani ya wilaya hiyo. Katika miradi yote aliyotembelea, alisisitiza kuwa kasi ya ujenzi inapaswa kuongezeka, kwani serikali imeshatoa fedha, na kinachohitajika kwa sasa ni utekelezaji wa haraka na kwa ufanisi.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Samaka ndugu Eliufoo Mandahu alieleza kuwa kasi ya ujenzi inaendelea polepole kutokana na fundi aliyepatikana kupitia mfumo wa NeST kufanya kazi taratibu na kukiuka mkataba uliomtaka kuwa na mafundi wa kutosha.
Aliongeza kuwa iwapo mafundi wataongezwa, ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa na matundu sita ya vyoo unatarajiwa kukamilika ifikapo tarehe 20 Machi 2025 na kuanza kutumika. Mradi huo una thamani ya shilingi 79,200,000, huku chanzo cha fedha kikiwa ni mpango wa BOOST.
Miradi mingine iliyotembelewa ni ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa katika Shule ya Msingi Dadu, wenye thamani ya shilingi 50,000,000, fedha zikitoka Serikali Kuu. Aidha, katika shule za msingi Kintandaa na Mnang’ana, ujenzi wa madarasa mawili na matundu sita ya vyoo kwa kila shule unaendelea, kwa gharama ya shilingi 58,600,000, huku chanzo cha fedha kikiwa pia ni mpango wa BOOST.
Mkurugenzi Msigala amesisitiza kuwa wahusika wa miradi hiyo wanapaswa kuhakikisha ujenzi unakamilika kwa wakati ili wanafunzi wanufaike na mazingira bora ya kujifunzia.
MWISHO
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa