Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju, leo Juni 2, 2025, amezindua kitini cha wawezeshaji kuhusu majadiliano ya mila na desturi katika jamii. Uzinduzi huo umefanyika katika Kata ya Ighombwe, Wilaya ya Ikungi, mkoani Singida.
Akizungumza kwa niaba ya Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii jinsia wanawake na makunfu maalumu Mheshimiwa Mwanaidi Ally,
Wakili Mpanju aliishukuru taasisi ya Amani Girls kwa mchango wake mkubwa katika kuwawezesha wanawake na wasichana, pamoja na kuendeleza maendeleo ya jamii kwa ujumla. Alilipongeza shirika hilo kwa kazi nzuri ya kuelimisha jamii kuhusu haki na nafasi ya mtoto wa kike.
Katika hotuba yake, Wakili Mpanju alisisitiza umuhimu wa kuhifadhi na kuenzi mila, desturi na tamaduni nzuri, huku akitoa wito wa kukemea na kuachana na zile zenye madhara kwa jamii.
"Mila na tamaduni ni sehemu ya utambulisho wa jamii. Tunapaswa kuziendeleza zile zinazojenga mshikamano, lakini zile zinazowanyima haki watoto, wanawake au makundi mengine hazifai kuendelea," alisema.
Aliwahamasisha wananchi kujiunga katika vikundi vya kiuchumi ili waweze kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayitolewa kwenye mapato ya ndani ya halmashauri yenye masharti nafuu kwa wanawake, vijana, wazee na watu wenye ulemavu.
"Nia ya Serikali ya Awamu ya Sita ni kuhakikisha maendeleo yanawafikia watu wote hadi ngazi ya chini kabisa. Wananchi mnatakiwa kuzitumia fursa hizi kujikwamua kiuchumi," aliongeza.
Aidha, alisema kuwa Benki ya NMB nayo inatoa mikopo kwa wafanyabiashara wadogo kwa masharti nafuu, na akawahimiza wananchi kuitumia kama mtaji wa kuanzisha au kukuza biashara zao.
"Tuchangamkie fursa ya mikopo. Tukopeshwe, tufanye biashara na tuongeze kipato chetu," alihimiza.
Kwa upande wake Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii, Bi. Haika Masawe, alisema kuwa Halmashauri imeanza kutoa mikopo kwa kila kundi la wanawake vijana na walemavu. Alieleza kuwa wanufaika wa mikopo wanapaswa kuunda vikundi vya kuanzia watu watano. Kwa upande wa vijana, wanakikundi wanapaswa kuwa wenye umri kati ya miaka 18 hadi 45.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa