kungi, Machi 4, 2025
Katika kuelekea maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Bi. Mariam A. Haroun, amemwaga sifa tele kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akitambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya nchi.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Mariam, ambaye ni mmoja wa viongozi wanawake waliobobea katika sekta ya manunuzi na ugavi, amepongeza juhudi za Rais Samia kwa kuimarisha sekta hiyo na kuongeza uwazi katika mifumo ya ununuzi wa umma.
Mariam amewahi kushika nyadhifa mbalimbali za uongozi, zikiwemo Mratibu wa Nchi katika Shirika la AMCA, linalojihusisha na tafiti mbalimbali, hususan kuhusu magonjwa ya mama na mtoto; Meneja wa Ghala katika Kampuni ya Resolute Mining; Mkaguzi Mkuu katika taasisi ya kifedha Abagamba Kamoi SACCOS; na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Manunuzi na Ugavi wilayani Monduli.Kwa mujibu wa Mariam, uongozi wa Rais Samia umeleta mabadiliko chanya, hasa katika sekta ya manunuzi na ugavi kupitia mfumo mpya wa kisasa.
"Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kuanzisha Mfumo wa Manunuzi wa Taifa (NEST), ambao umeongeza uwazi na kurahisisha mchakato mzima wa manunuzi. Mfumo huu utasaidia vijana wa kike na wa kiume kujiajiri na kujitegemea kiuchumi," alisema Mariam.
Aidha, aliwahimiza wanawake kujitokeza kwa wingi kushika nafasi za uongozi, akisisitiza kuwa wanawake wana uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii na uchumi wa taifa.
"Tunahitaji kuona wanawake wengi zaidi wakiongoza katika sekta mbalimbali. Hakika tunaweza!" alisisitiza.
Kwa kumalizia, Mariam alimtakia Rais Samia heri na baraka ili aendelee kuongoza taifa kwa mafanikio makubwa zaidi.
"Tunaendelea kumuombea Mheshimiwa Rais, ili aendelee kutuongoza kwa hekima na busara," alisema.
Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa kila mwaka tarehe 8 Machi kwa kutambua mchango wa wanawake katika jamii, siasa, na uchumi, pamoja na kuhamasisha usawa wa kijinsia katika sekta zote.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa