Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego ameongoza ukaguzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani Ikungi, akiwa ameambatana na Katibu Tawala wa Mkoa Dkt. Fatuma Mganga pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na Wilaya ya Ikungi, ikiwa ni maandalizi ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2025.
Katika sekta ya elimu, viongozi hao wametembelea mradi wa ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Samamba (Utaho 'A') unaogharimu shilingi milioni 544.2 fedha zilizotolewa na Serikali Kuu.
Kwa upande wa maji, ukaguzi umefanyika katika mradi wa maji wa Utaho 'A' unaogharimu shilingi milioni 300 ukitekelezwa kwa ufadhili wa wahisani. Aidha, mradi mwingine wa maji eneo la Wibia umehusishwa pia, wenye thamani ya shilingi milioni 60 ukifadhiliwa na Serikali Kuu.
Katika sekta ya afya, ujenzi wa walkways katika Hospitali ya Wilaya ya Ikungi umeangaliwa kwa makini. Mradi huo wa thamani ya shilingi milioni 195 umetekelezwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu na utatembelewa na Mwenge wa Uhuru.
Miradi ya barabara pia imechukua nafasi muhimu, ambapo barabara inayosimamiwa na TANROADS pamoja na ile mpya ya TARURA zimetembelewa ili kuhakikisha maandalizi yanaendelea kwa kasi na ubora unaotakiwa kabla ya ujio wa Mwenge wa Uhuru.
Kwa upande wa maendeleo ya vijana, viongozi hao wametembelea mradi wa Kikundi cha “Ikungi Boys” ambao umetekelezwa kwa gharama ya milioni shilingi 10 kwa mchango wa Halmashauri.
Katika eneo la utawala, ujenzi wa jengo la ofisi ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) umeangaziwa, mradi unaogharimu shilingi milion 263 ukiwa umefadhiliwa na Serikali Kuu.
Akizungumza baada ya ukaguzi, Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego amesema kuwa miradi hii iendane na mahitaji ya wananchi waliopo katika eneo husika ili iwe na tija na kuleta matokeo chanya katika maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe.Thomas Apson ameshukuru na kusema kuwa ukaguzi wa miradi katika Wilaya ya Ikungi umeonesha dhamira ya dhati ya Serikali ya mkoa wa Singida katika kusimamia maendeleo ya wananchi kupitia miradi ya afya, elimu, maji, vijana na miundombinu.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa