Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ndugu Kastori Msigala akiongozana na wakuu wa Idara na vitengo awataka wasimamizi wa miradi mbalimbali inayotekelezwa katika Wilaya ya Ikungi kusimamia kwa karibu na kwa uadilifu ili iweze kukamilika kwa wakati na kuanza kutumika.
Akizungumza wakati wa ziara yake hii leo Tarehe 19 Septemba, 2025 kata ya Ntuntu, Mkurugenzi Mtendaji amesema kuwa, hayupo tayari kunyamaza panapotokea ucheleweshwaji wa miradi kutokana na uzembe wa watu wachache.
"Fedha zinapotoka huja na maelelekezo ya lini mradi unapaswa kuanza na lini unapaswa kukamilika hivyo panapotokea ucheleweshwaji ni uzembe na tunapaswa kuwachukulia hatua za kisheria" amezungumza Msigala
Hata hivyo amewataka walezi wa kata zote kutembelea miradi yao na kujua maendeleo na changamoto zilizopo ili ziweze kutatuliwa kwa lengo la kuhakikisha miradi inakamilika haraka na kwa ubora kulingana na maelekezo ya serikali.
Mkurugenzi Msigala amefanya ziara hiyo kukagua hali ya ukamilishaji wa jengo la Mama na Mtoto kituo cha afya Ntuntu kupitia fedha za Halmashauri milioni 25 na mradi huo upo hatua za ukamilishaji, mradi wa ujenzi wa madarasa mawili matundu sita ya vyoo shule ya msingi Ntewa unaogharimu milioni 57.2 kupitia fedha za BOOST na mradi huo upo hatua za awali.
Pia ametembelea na kukagua ujenzi wa madarasa mawili, matundu sita ya vyoo shule ya msingi Taru, mradi unaogharimu milioni 57.2 kupitia fedha za BOOST na ujenzi huo upo hatua za Ukusanyaji wa mchanga, kokoto na mawe.
Katika shule za msingi Lighwa na Ujaire ujezi wake upo hatua za awali ambapo Mkurugenzi Msigala ameagiza miradi hiyo kuanza mara moja kwani fedha tayari zimeingia kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa