Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Mhe Thomas Apson apokea taarifa ya uwepo wa ugonjwa wa kipindupindi katika kata ya Mgungira kijiji cha Ufana na kata ya Mwaru kijiji cha Kaugeri pamoja na maeneo yaliyokaribu na bwawa la kuvua samaki Wembere.
Akizungumza katika kikao cha PHC katika ukumbi wa Halmashauri
Mkuu wa Wilaya ameagiza kufungwa kwa bwawa la uvuvi wa samaki la Wembere lililopo maeneo yanayozunguka kata ya Mgungira ili kuepusha kuenea kwa ugonjwa huu katika maeneo mengine kuzunguka eneo hilo.
Hata hivyo timu ya wahudumu wa afya wanaendelea kutoka matibabu kwa watu wenye viashiria vya ugonjwa huo wa kipindupindu na kutoa rai kwa wananchi kutumia maji Safi na salama majumbani, na kunawa maji tiririka na sabuni mara watokapo chooni.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Victorina Ludovick, Mkurugenzi Mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Katibu Tawala Wilaya ya Ikungi, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya pamoja Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Ikungi wameungana kujadili mlipuko huo huku wakiunga mkono mawazo ya kitaalamu ya watoa huduma wa afya pamoja na maagizo ya Mkuu wa Wilaya ya kufunga bwawa pamoja na kuchimbwa visima vya maji Safi na salama, ujenzi wa vyoo bora katika maeneo hayo kunusuru adha iyo kwa haraka.
Akisoma taarifa hiyo Afisa Afya Brayson Shoo amesema kuwa Kipindupindu ni ugonjwa unaosababishwa na vimelea vinavyoshambulia mfumo wa chakula na kusababisha kuharisha majimaji yanayofanana na maji ya mchele na huweza kuambatana na kutapika hivyo kupoteza maji mengi mwilini.
Ameongeza na kusema kuwa ugonjwa huu unaambukizwa kwa kula vyakula au kunywa maji yaliyochafuliwa au yenye kinyesi cha binadamu chenye vijidudu au vimelea vinavyoeneza Kipindupindu.
Mwisho wataalamu wa afya wameomba kuongezewa dawa, vifaa tiba, vitendanishi na mahitaji mengine muhimu katika kambi ya kipindupindu kwa haraka kufanya juhudi za kunusuru hali hiyo Katika kata ya Mgungira na Mwaru Wilayani hapa.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa