Watendaji wa vijiji wasioweza kutimiza majukumu yao wametakiwa kuchukuliwa hatua za haraka, kauli hiyo imetolewa jana tarehe 18 June, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi, Ndugu Kastori Msigala, alipokuwa kwenye ziara ya kufuatilia na kukagua miradi ya maendeleo katika Kata ya Iglanson.
Msigala amesema Afisa Utumishi anatakiwa kuwachukulia hatua za haraka watendaji wote wa vijiji ambao wameshindwa kutekeleza majukumu yao ya kila siku huku wakiendelea kupokea mishahara, amesisitiza kuwa haiwezekani mtendaji wa kijiji kushindwa kusimamia na kukusanya mapato na kuruhusu biashara kufanyika kiholela, hali hii inafanya Halmashauri kukosa mapato ya ndani ambayo ni muhimu kwa maendeleo.
Akiwa katika Shule ya Msingi Mnyange, Msigala alionesha kusikitishwa na mtendaji wa kijiji kwa kushindwa kuchukua hatua kuhakikisha fedha zilizoingizwa kwenye akaunti ya kijiji zinatumika kumalizia ufungaji wa madirisha ya aluminium.
"Mtendaji unatakiwa kuwajibika, huwatendei haki watoto, serikali imetoa fedha kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na mazingira mazuri ya kusomea, kwa nini mpaka sasa hamjatafuta fundi kufunga madirisha?" alihoji Msigala
Katika ziara hiyo, ametembelea pia mradi wa ujenzi wa madarasa mawili katika Shule ya Sekondari Iglanson yenye thamani ya shilingi milioni 46, pamoja na ujenzi wa matundu nane ya vyoo yenye thamani ya shilingi milioni 14.4, na utengenezaji wa madawati 80 kwa gharama ya shilingi milioni 5.5
Katika ukaguzi huo, Ndugu Kastori amesisitiza kuwa mzabuni asilipwe malipo ya mwisho hadi pale atakapokamilisha marekebisho ya kasoro ndogo zilizopo ili mradi huo uendane na thamani halisi ya fedha iliyotolewa na serikali.
Aidha, amekagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Afya Iglanson kilichojengwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 500, kituo hicho kinahudumia zaidi ya wakazi 20,000 na kimejengwa kwa kutumia mfumo wa Force Account.
Akiwa kituoni hapo, amesisitiza kuboreshwa kwa huduma za afya, ikiwemo kuhakikisha mashine kubwa ya kisasa ya kufulia nguo inaanza kufanya kazi mara moja kwa kurekebisha miundombinu ya jengo la Laundri na mifumo yake ya mabomba.
"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametoa fedha nyingi ili huduma bora za afya ziwafikie wananchi hadi vijijini,hivyo ni wajibu wenu kuhakikisha mnawatendea haki wananchi kwa kuwapatia huduma bora za afya," alisisitiza Msigala.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa