Waziri wa Maji Mhe. Makame Mbarawa aahidi upatikanaji wa maji Wilaya ya Ikungi
Posted on: February 13th, 2019
Waziri wa Maji Mhe. Makame Mbarawa ameahidi kutoa fedha kwa ajili ya uchimbaji wa visima ishirini (20) na usambazaji wa maji ya bomba kata ya Ihanja na Iseke katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Ahadi hiyo ameitoa Februari 13, 2019 katika kituo cha Afya Ihanja kilichopo katika kijiji cha Ihanja kata ya Ihanja Wilaya ya Ikungi alipokwenda kutembelea kituo hicho ambacho kimekamilisha ujenzi wa majengo saba ya kutolea huduma mbalimbali za Afya.
Akijibu ombi la Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi Ndugu Justice Laurence Kijazi kuhusu upatikanaji wa maji Wilaya ya Ikungi Waziri Mbarawa amesema visima hivyo Ishirini vitachimbwa katika majimbo yote mawili ya uchaguzi ambapo Jimbo la Mashariki litapata visima kumi (10) na Jimbo la Magharibi pia litapata visima kumi (10).
Katika usambazaji wa maji ya bomba kijiji cha Ihanja na Iseke Waziri Mbarawa amesema kuwa atatoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa pampu na uwekaji wa umeme katika kisima cha Iseke ambapo fedha ziatakazotolewa ni za kununulia transforma na nguzo za umeme ili kufanikisha hilo amemtaka Mhandisi wa maji wa halmashauri ya wilaya ya Ikungi Ndugu Victor Kamote kuandaa makadirio ya ghrama za kazi hiyo na kuziwasilisha kwake haraka sana ili aweze kuzifanyia kazi.
Aidha katika mradi huo pia Mbuge wa Singida Magharibi Mhe. Elibariki Kingu ameahidi kutoa shilingi milioni Ishirini kutoka katika mfuko wa Jimbo na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Ikungi ndugu Ali Mwanga ameahidi Halmashauri itatoa shilingi milioni arobaini. Fedha hizo zitafanikisha kununulia mabomba ambayo yatatoa maji kutoka kisima kilichopo Iseke hadi maneo ya vijiji hivyo viwili ikiwemo kituo cha Afya Ihanja.
Awali akitoa taarifa ya hali ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Ikungi Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Ndugu Justice Kijazi amesema hali ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi sio ya kuridhisha. Akitoa takwimu za watu wanaopata maji safi na salama Mkurugenzi Kijazi amesema Idadi ya wakazi wanaopata maji safi na salama ni 126,195 ambao ni sawa na asilimia 40.1 tu ya idadi ya watu wote 309,031(projection 2019 kutokana na sense ya 2012) wa Wilaya ya Ikungi. Ndugu Kijazi ameongezea kusema kuwa wakazi wengi wa Wilaya ya Ikungi wanategemea vyanzo vya maji ambavyo si salama na mara nyingine sio vya uhakika.
Pia amesema baadhi ya wakazi hulazimika kutembea umbali mrefu na kutumia muda mwingi kufuata maji ya kutumia majumbani.
Katika kukabiliana na hali ya ukosefu wa maji Mkurugenzi Mtendaji alimweleza Waziri kwamba mkakati uliopo ni kwa Halmashauri ya Wilaya imepanga kujenga na kukarabati miradi ya maji katika vijiji vya Mtunduru, Ighuka, Isuna, Sambaru, Mnane, Mkunguakihendo, Iseke na Sakaa katika mwaka wa fedha 2018/2019.
Hata hivyo Mkurugenzi huyo aliongeza kusema pamoja na malengo hayo ya upatikanaji wa mji Halmashauri ya Wilaya inachangamoto zinazokwamisha kutekeleza kwa ufanisi kwa miradi. Changamoto hizo ni pamoja na fedha za miradi ya maji kutofika kwa wakati kutoka Wizarani kama ilivyopangwa. Idara ya maji ya Halmashauri ya Ikungi kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha kama gari kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji utekelezaji wa miradi, ukosefu wa vifaa vya kufanyia utafiti (survey) vifaa vya kupima ubora wa maji na vifaa kwa ajili ya ukarabati wa pampu na mabomba.
Waziri Makame Mbarawa alifika katika kituo cha Afya cha Ihanja kukagua tatizo la upatikanaji wa maji kituoni hapo akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Singida. Katika ziara hiyo pia alifika kijiji cha Ulyampiti kuona chanzo cha maji ya bomba yanayosambazwa kijijini hapo. Katika msafara wake aliongozana na Mwenyekiti wa bodi ya maji Mkoa wa Singida Ndugu Deocres Kamara na wataalamu mbalimbali wa sekta ya maji na Afya kutoka Mkoa wa Singida.