Baraza la Wafanyabiashara Wilaya ya Ikungi limekutana leo Alhamisi, Novemba 27, 2025, katika Ukumbi wa Halmashauri, likiwa na lengo la kujadili namna ya kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza mapato ya serikali.

Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mhe. Thomas Apson, Afisa Mazingira, Bw. Richard Rwehumbiza amesema kuwa biashara ndiyo chanzo muhimu cha mapato ya serikali, hivyo ni vyema elimu juu ya umuhimu wa kulipa kodi na leseni kutolewa kwa wafanyabiashara ili kuchochea maendeleo ya wilaya.
“Biashara ndiyo inaleta mapato ya serikali. Hivyo elimu ya kodi na leseni ni muhimu ili tuweze kupata maendeleo ya kweli,” amesema Rwehumbiza.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ikungi, Ndg. Niceforus Mgaya, amesema kuwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 imeainisha biashara na uwekezaji kama nguzo muhimu ya uchumi wa nchi na kuongeza kuwa ni muhimu wafanyabiashara kushirikiana na maafisa wa halmashauri kwa hekima na busara, huku akiahidi kuboresha mifumo ya mawasiliano ili kuwasaidia wafanyabiashara kukumbushwa kwa wakati kuhusu wajibu wao.

Pia, Afisa Biashara , Bi. Mariam Abdallah, amewataka wafanyabiashara kuhakikisha wanalipia leseni zao mapema na kuwakumbusha wafanyabiashara wa masuala ya burudani kujisajili kupitia mfumo wa AMIS – BASATA ili kurahisisha taratibu za uendeshaji wa shughuli zao.
Naye Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wilaya ya Ikungi, Ndg. Kurwa Shilinde, amesema ni wakati muafaka kwa halmashauri kusaidia katika kuainisha fursa za biashara, kutenga maeneo ya uwekezaji, pamoja na kutoa elimu ya mara kwa mara ili kuwawezesha wafanyabiashara kutimiza wajibu wao katika kuisaidia serikali kuboresha uchumi wa wilaya.
Ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi
Anuani ya Posta: S.L.P 42, Singida, Tanzania
Simu ya mezani: +255262964037/6
Mobile:
Barua pepe: ded.ikungidc@singida.go.tz
Hakimiliki @2017 Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi. Haki zote zimehifadhiwa